: MAOMBI YA KUTUBU KWA AJILI YA CHANZO CHA MAGONJWA UNAYOTAKA YAONDOKE KWAKO AU KWA UNAOWAOMBEA.









Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 
Katika maombi yetu ya kufunga siku tatu tunaanza na Kipengele muhimu sana  yaani Maombi ya kutubu kwa ajili ya chanzo cha ugonjwa ambao tunataka uondoke.

Kwanini tutubu kwa ajili ya chanzo cha ugonjwa tunaotaka uondoke?

Ni kwa sababu magonjwa yote kwenye ulimwengu wa roho hupita katika mlango hata kuingia ndani ya mtu.
Milango ni mingi baadhi ya milango ni dhambi, uzembe wa maombi, mapigo, uonevu wa shetani, kurogwa, kuambikizwa n.k

■Ukisoma  Hesabu 14:11-12 unaona kwamba Waisraeli kwa sababu ya kumdharau MUNGU na kutokumuamini  kulipelekea MUNGU atake kuwaangamiza kwa Magonjwa aina ya tauni.
Biblia inasema " BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa WATANIDHARAU HATA LINI? WASINIAMINI HATA LINI? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao. NITAWAPIGA KWA TAUNI, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao."

Nini tunajifunza kutoka kwa Waisraeli?

Dharau yao na kutokumwamini MUNGU kulifungulia mlango wa magonjwa magonjwa kuingia kwao.

 ■Ukisoma 1  Yohana 3:8 Biblia inasema ''atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

Kumbe anayetenda dhambi ni mali ya shetani maana Biblia inasema atendaye dhambi ni wa Ibilisi  na Ukisoma Yohana 10:10a Biblia inasema "Mwivi(Shetani) haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; ......." 

Kumbe shetani kazi yake ni kuiba na kuua na kuharibu,  hivyo ukiwa mtenda dhambi ujue wewe ni wa shetani na shetani anaweza kutimiza hayo yaliyo yake ambayo ni  kuiba, kuharibu na kuua. Na hayo anaweza kuyatimiza kwa njia nyingi ni mojawapo kwa njia za magonjwa anayoyalete yeye shetani kupitia wachawi na mawakala wake wengine.

■Kuna Magonjwa mengine hutokana pia na maovu ya wanadamu mbele za MUNGU. 
Mfano hai ni huu 

Yeremia 21:6 "Nami NITAWAPIGA wenyeji wa mji huu, wanadamu na wanyama pia; WATAKUFA k3wa TAUNI KUBWA."

Hata ukisoma Ezekieli 6:11 Biblia inasema  "Bwana MUNGU asema hivi; Piga kwa mkono wako, ipige nchi kwa mguu wako, ukaseme, Ole! Kwa sababu ya machukizo maovu yote ya nyumba ya Israeli; maana wataanguka kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni."

Biblia inasema kwa sababu ya machukizo ya watu vita, njaa na magonjwa yataachiliwa ili kuua watu.

 ■Kuna wengine pia katika kuumwa hukosea zaidi kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao wanatumia uchawi kuagua, huko ni kuitafuta mauti.
Ona mfano huu 

2 Nyakati 16:12-13 " Akashikwa Asa na ugonjwa wa miguu katika mwaka wa thelathini na kenda wa kumiliki kwake; ugonjwa wake ukazidi sana; lakini hakumtafuta BWANA katika ugonjwa wake, bali waganga. Asa akalala na babaze, akafa katika mwaka wa arobaini na mmoja wa kumiliki kwake."

Huyu Asa alikufa kwa sababu hakumtafuta MUNGU.

Ndugu yangu, ukihitaji upone ugonjwa mhitaji MUNGU ukianza na maombi ya toba juu chanzo cha ugonjwa huo unaotaka uondoke.

Narudia tena, ndugu yangu, ukihitaji upone ugonjwa mhitaji MUNGU ukianza na maombi ya toba juu chanzo cha ugonjwa huo unaotaka uondoke.

Inawezekana chanzo cha ugonjwa huo ni kulogwa, tubu kwa ajili ya makosa yako yaliyowapa uhalali wachawi kukuloga.

Inawezekana chanzo cha ugonjwa wako ni uonevu wa shetani,  tubu kwa ajili ya makosa yako yaliyompa shetani uhalali wakukuonea.

Inawezekana ugonjwa wako unatokana na laana,  tubu kwa ajili ya uhalali wa laana hiyo kukupata.

Inawezekana chanzo cha ugonjwa wako na hila za watu au ni maambukizi wakati ukifanya dhambi, ndugu ukihitaji kupona anza na kutubu kwanza juu ya kilichopelekea wewe kuumwa.

Kuna magonjwa mengine chanzo chake hukufuata Kanuni za kiafya, tubia chanzo kilichopelekea ugonjwa huo kwako.

Kuna magonjwa ni mishale ya kuzimu inayorushwa duniani, kama mshale huo umekupata tubu na Bwana YESU KRISTO ataung'oa mshale huo uondoke kwako.

 Nini ufanye kwenye maombi?

1  Kuna magonjwa mengine  kupona kwake anza na Maombi ya toba kwanza maana dhambi au makosa ndio chanzo cha ugonjwa huo, tubu kwa ajili ya chanzo cha ugonjwa na MUNGU atakusamehe na kukuponya au atamsamehe na kumponya huyo unayemuombea.

Mathayo 9:2 "Na tazama, WAKAMLETEA MTU MWENYE KUPOOZA, amelala kitandani; naye YESU, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO."

2  Tubu kwa ajili ya chanzo cha ugonjwa.

Danieli 9:13 "Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, MABAYA HAYA YOTE YAMETUPATA lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ILI TUGEUKE NA KUYAACHA MAOVU YETU, NA KUITAMBUA KWELI YAKE."

3. Tubu ili MUNGU akusamehe, na kuna magonjwa huondoka baada ya mtu kusamehewa na MUNGU. 

  Zaburi 103:3-4 " Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,  Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,"

4. Omba maombi ya toba na kujitakasa maana maombi hayo yanaweza kuondoa uhalali wa magonjwa eneo hilo.

Isaya 33:24 "Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao."
Omba ndugu kwa imani.
Omba katika jina la YESU KRISTO  na utasamehewa na kuponywa magonjwa. 

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kueleea naamini  ameelewa .

Hapa chini ni MAOMBI YA KUTUBU KWA AJILI YA CHANZO CHA MAGONJWA UNAYOTAKA YAONDOKE KWAKO AU KWA UNAOWAOMBEA.
Maombi haya ni kwa ajili ya mtu ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba.

Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.

MAOMBI YA KUTUBU KWA AJILI YA CHANZO CHA MAGONJWA UNAYOTAKA YAONDOKE KWAKO AU KWA UNAOWAOMBEA.


Baba MUNGU wa Mbinguni  hakuna  aliye kama wewe.

Niko niko mbele zako BWANA ninaomba unisamehe dhambi zangu zote,  maovu yangu yote na makosa yangu yote. 

Ninakuomba MUNGU Baba unisamehe dhambi ninazozikumbuka na dhambi ambazo sizikumbuki.

Eee Bwana YESU KRISTO Mwokozi ninakupokea kwa upya leo ili uwe Bwana na Mwokozi wangu. 

Eee Bwana YESU KRISTO Mwokozi ninakuomba ulifute jina langu katika kitabu cha hukumu na katika vitabu vyote vya kuzimu, na nakuomba sasa Bwana YESU KRISTO uliandike jina langu katika kitabu chako cha uzima.

Kuanzia leo ninamkataa shetani na kazi zake zote, katika jina la YESU KRISTO. 

Kuanzia leo ninaufunga ukurasa wa dhambi katika maisha yangu, na naufungulia sasa ukurasa wa mema tu ayatakayo MUNGU Baba wa Mbinguni. 

Eee MUNGU Baba niko mbele zako nikitubia dhambi zangu zote  zilizofungulia mlango wa ugonjwa (utaje) ili uje kwangu, ninatubu BWANA nikiomba unisamehe. 

Ninatubia makosa yangu na maovu yangu yaliyosababisha ugonjwa huu(utaje) kuingia kwamba, ninaomba unisamehe Eee MUNGU Baba wa Mbinguni. 

Kuna mahali sikukusikiliza ndio maana nikajikuta matatizoni,  kuna wakati sikufanyia kazi maelekezo yako ndio maana shetani akapata nguvu za kunitesa, ninatubu mbele zako MUNGU Baba ninaomba unisamehe na unilinde ili shetani asinitese  tena.

Kuna wakati sikuwa mwaminifu katika kutoa zaka na dhabihu ikafungulia mlango wa matatizo kwangu   au Kwa familia yangu  na moja ya matatizo hayo ni magonjwa ya mlipuko yanayoipata dunia,  ninatubu  MUNGU Baba naomba unisamehe. 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi,  wewe ulipomponya mtu aliyepooza ulianza kwa kumsamehe dhambi. 
Neno lako linasema katika Mathayo 9:2  kwamba "Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye YESU, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako."

Nami Bwana YESU ninaomba unisamehe dhambi zangu ili nipate kupona. 
Ukinisamehe wewe hakika ninapona.

Eee MUNGU Baba ninakusihi unisamehe ili nipate kupona.
Neno lako linasema kwamba ukinisamehe utaniponya na kuukomboa uhai wangu dhidi ya kaburi, ndivyo Zaburi 103:3-4 inavyosema kwamba " Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,  Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,"

Eee MUNGU Baba ninatubia kila chanzo cha ugonjwa kwangu na ninatubu kwa ajili ya chanzo cha tatizo langu lolote maana nimetambua kwamba nikitubu ukanisamehe unaniponya pia.

Ninaomba Baba wa Mbinguni unisamehe na unipe neema ya kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO Mwanao mpendwa.

Eee MUNGU Baba ninaomba unirehemu na uniponye ili nami nifike hatua niseme kwamba hakuna ugonjwa kwangu na kwa familia yangu kama Neno lako linavyosema katika Isaya 33:24 kwamba  "Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao."

Ninakushukuru MUNGU Baba maana umenisamehe na kunipa wokovu wako katika KRISTO. 
Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kuamini na kupokea.
Amen amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen. 

Hakika umeshinda.
Endelea na Maombi ndugu, usiishie maombi haya tu bali omba zaidi maana haya yalikuwa maombi ya kuanzia tu.
MUNGU akubariki sana. 
By Peter Mabula. 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 
+255714252292.
Omba ndugu na utamuona MUNGU wa Miujiza. 
Ubarikiwe

Comments

Popular Posts