HARIBU MAJINI MAHABA YA NDOTONI.

BWANA  YESU asifiwe ndugu.
Karibu tuzibomoe ngome za shetani ambazo hutenda kazi ndotoni hadi hadharani.

Ndugu mmoja aliniuliza swali ambalo ndilo lilipelekea MUNGU kunipa ujumbe huu, ndugu huyo aliuliza kwamba '' Naota mara kwa mara nafanya mapenzi na watu tofauti tofauti ndotoni, watu hao wengine nawafahamu na wengine siwafahamu naomba unisaidie kujua maana yake na jinsi ya kuzuia jambo hili ambalo hunifanya nijichafue kila siku, na wakati mwingine nikiamka nakuta dalili zote za kwamba nilifanya mapenzi muda mfupi uliopita, na hata uchovu nakuwa nao. UBARIKIWE''

 BWANA YESU asifiwe.
Ngoja nikufundishe jambo hili kuhusu ndoto hizo chafu.


Ukiota unafanya mapenzi ndotoni maana yake una jini mahaba au jini maimuna. Yaani kama wewe ni mwanamke basi una mme wa rohoni ambaye ni jini na kama wewe ni mwanamume basi tambua kwamba una mke wa rohoni wa kipepo ambaye siku akitaka kuja huja na wewe unaona ni ndoto kumbe alikuja na kufanya ngono na wewe  na haya yanatokea kwa mtu ambaye hana ulinzi wa damu ya YESU KRISTO. 

Kuna aina 3 za mashetani.

1. shetani mwenyewe.
2. wakuu wa idara za kipepo.
3. watenda kazi.

maimuna ni mmoja wa wakuu wa vitengo wa shetani, na kitengo chake ni kuleta ukahaba kwa wanadamu. Watenda kazi ni majini hawa wa kawaida ambao hutumwa na maimuna kuja kufanya ukahaba na wanadamu ambao hawana ulinzi wa damu ya YESU KRISTO. maimuna anaweza kutuma jini la kike kwa ajili ya kwenda kufanya mapenzi na wanadamu wanaume na  na kama mwanadamu aliyekusudiwa ni mwanamke basi hutumwa jini la kike. na majini yote ya ukahaba yanaitwa maimuna na wakati mwingine kwa sababu majini haya ni viumbe wa kiroho huweza kuwaingia watu kabisa na kuwatumikisha kipepo. Ndio maana wengi tumewaombea na mapepo yakiwa yanatoka husema wao ni maimuna, ukisikia hivyo wewe mtumishi wa MUNGU tambua kwamba unayemuombea alikuwa anateswa na jini mahaba au jini maimuna. maimuna ni ukoo wa majini mahaba yote ndio maana nimewahi kumwombea mtu nikiwa Zanzibar akiwa anateswa na jini mahaba au maimuna na hata hapa Dar nimewahi kumwombea Dada mmoja ambaye naye alikuwa na jini mahaba, hivyo unaweza kushangaa kwamba jini mahaba wa Zanzibar kafikaje Dar kumbe jina hilo maimuna ni jina la ukoo wa majini yote ya ukahaba. 
mapepo haya yakimwingia mtu mtu huyo hubadilika mara moja. Kama mme au mke alikuwa mwaminifu kwenye ndoa yake basi yakimwingia haya majini mahaba huanza kutokuridhika na mwanandoa mwenzake na kuanza kutoka nje ya ndoa, ni hatari sana . 
Wapo wadada wengi hujiuza miili yao, chanzo ni jini mahaba aliyewaingia.Ndugu yangu ukiota ndoto za kufanya mapenzi mara kwa mara kemea sana jambo hilo kwa maombi ya vita kupitia jina la YESU KRISTO. Yohana 8:36 Biblia inasema ''BWANA YESU akikuweka huru , utakuwa huru kwelikweli.''
 
Kuna madhara makubwa kwa mtu kuwa anafanya mapenzi na majini ndotoni. Madhara ni kwamba mtu huyo 

-Atakuwa ameingia agano na mashetani.

-Atakuwa anatumikishwa na mashetani.

- Majini hayo unayofanya nayo mapenzi huzuia wewe kuoa au kuolewa.

-Majini hayo hufukuza wachumba kipepo. unashangaa kila ukipata mchumba siku chache baadae kabla hata uchumba wenu haujatangwazwa kanisani anakuona mbaya na kuanza kujuta kwamba alikosea kuchagua kumbe jini mahaba yuko katikati yenu.


-Majini haya hushirikiana na jini shamsuh ambalo ni jini la kujibadilisha sura, yaani kama mkeo/mmeo ulimuona mzuri sana mwanzo baada ya jini maimuna kuanza kufanya mapenzi na wewe kwa njia ya ndoto na kuweka ngome ya kudumu kwako jini shamsuh huingia usoni mwa mmeo au mkeo na wewe unaanza kumuona mbaya sana na wakati mwingine unaanza kujuta kwanini ulimuoa huyo. Unaweza kujiuliza kwamba zamani ulimpenda sana mmeo au mkeo lakini siku hizi humpendi tena kumbe jini maimuna kwa kushirikiana na jini shamsuh wako kazini kuhakikisha ndoa yao inakufa, kuhakikisha uchumba wako unaharibika. Ndio maana MUNGU kwa upendo wake wa ajabu alimtoa Mwanaye ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele-Yohana 3:16.
 
Ndugu yangu ukitaka majini yasifanye mapenzi na wewe kwa njia ya ndoto basi 
-hakikisha unampokea BWANA YESU kuwa BWANA na MWOKOZI wa maisha yako na baada ya hapo 
-uwe mtu wa vita yaani mwana maombi  na tena 
-hakikisha kila siku kabla ya kulala unaomba maombi kwamba damu ya YESU KRISTO ikuzingire pande zote maana Tunamshinda shetani kwa damu ya Mwana kondoo YESU KRISTO-uFUNUO 12:11.
 Na kwa sababu ya uonevu wa shetani na majini yake kuzidi sana duniani '' Kwa kusudi hili BWANA YESU alidhihilishwa ili azivunje kazi zote za shetani- 1 Yohana 3:8b.
 
Ndugu unayeteswa na ndoto hizo za kufanya mapenzi mara kwa mara kimbilia kwa YESU na utapona yeye BWANA YESU anasema '' Njoni kwangu nini nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha-Mathayo 11:28.
 JIFUNIKE KWA DAMU YA YESU SIKU ZOTE KWA MAOMBI HAYA.

BWANA MUNGU Ninakushukuru Kwa Kunilinda, Asante Kwa Damu Ya Mwanao YESU KRISTO Inenayo Mema Siku Zote. Najifunika Kwa Damu Ya YESU KRISTO, Ninawafunika Ndugu Zangu Wote Kwa Damu Ya YESU KRISTO, Nafunika Familia Yangu, Ndugu Zangu, Nyumba Yangu, Biashara Yangu, Ofisi Yangu, Chakula Changu, Fedha Zangu, Kiwanja Changu, Rafiki Zangu, Majirani Zangu Huduma Yangu Na Kila Kinachonihusu Kwa Damu Yenye Nguvu Ya YESU KRISTO Wa Nazareth. Ninalifunika Anga Lote, Nchi Yote Na Bahari Yote Kwa Damu Ya YESU KRISTO. Imeandikwa Katika Ufunuo 12:11 " Nao Wakamshinda(shetani) Kwa Damu Ya Mwana Kondoo(YESU) Na Kwa Neno La Ushuhuda Wao" Ewe shetani, Nimeitumia Damu Ya YESU KRISTO Kukushinda Sasa Na Hata Milele Katika Jina La YESU KRISTO, jini mahaba nakutetekeza kwa jina la YESU KRISTO maana Neno la MUNGU katika Yeremia 1:10 kwamba MUNGU ameniweka juu ya falme zote za mashetani ili kuwang'oa mashetani, na kuwabomoa na kuwaharibu na kuwaangamiza kwa jina la YESU KRISTO.  Sasa nawaangamiza majini wote waliotumwa kwangu kutoka kuzimu kwa jina la YESU KRISTO Amen.



Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Baraka  Audax
Injili ya Kristo  Zanzibar.
0717461006
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
MUNGU Akubariki.

Comments

Popular Posts